Thursday, January 22, 2015

Mvua kubwa yasababisha mafuriko na kuharibu makazi ya watu mkoani Mtwara.Nyumba ambazo idadi yake haijaweza kufahamika mara moja zimebomoka na zingine kuingiwa na maji, miti kuanguka ovyo huku pia baadhi ya barabara katika manispaa ya Mtwara/mikindani zikijaa maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Mtwara.
ITV ilifika kwenye eneo la magomeni bomba la bure na kukuta baadhi ya wakazi wake wakihangaika kuyatoa maji yaliyoingia ndani ya makazi yao kutokana na mvua hiyo kunyesha siku mzima kuanzia usiku wa manane, huku maeneo mengine yakishuhudiwa wakazi wake wakihangaika kuhamisha vifaa vya ndani kuyakimbia mafuriko hayo.
 
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo la Magomeni Bomba la bure wamedai wamepata hasara kubwa kutokana na mafuriko hayo na kwamba yanasababishwa na barabara mpya ya chuno kuelekeza mifereji yote  ya maji kwenye makazi yao na hakuna jitihada zo zote za serikali kuwasaidia kuondokana na tatizo hilo.
  
Kwenye maeneo ya Skoya na Kyanga ITV ilishuhudia barabara zimefunikwa na mafuriko na magari yakipita kwa taabu huku wakazi wa maeneo hayo wakiiomba serikali kuwalipa fidia ya hasara na mali zao kwa kuwa mafuriko hayo yamekuwa yakijirudia rudia na serikali imeshindwa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Viongozi wa Sudani kusini wakubaliana kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.Jitihada za Tanzania za kusaidia kuleta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Sudani kusini kwa njia mazungumzo umeanza kuonyesha mwelekeo wa mafanikio baada ya viongozi wa makundi matatu yaliyotofautianandani ya chama cha (SPLM) kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo.
Wakizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo mbele ya marais Mh. Uhuru Kenyeta wa Kenya, Yoweri Museven wa Uganda na mwenyeji wao Mh Rais Dr, Jakaya Kikwete viongozi makundi yote yaliyotofautiana wameahidi mbele ya marais Dr, Jakaya Kikwete wa Tanzania, kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa.
 
Kwa upande wao rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda wamewataka viongozi wa makundi hayo kuona umuhimu wa kutanguliza mbele maslahi ya wananchi wao wanaoendelea kuteseka kwa sababu ya tofauti za mitazamo ambazo zinaweza kumalizika bila  kupigana, na wameipongeza Tanzania kwa kuendeleza harakati za hayati baba wa taifa Mwalim Nyerere za kumaaliza matatizo kwa njia za mazunguzo.
 
Awali mwenyekiti wa mazungumzo hayo Mh John Malechelea na katibu wa CCM iliyokuwa inaratibu zoezi hilo Mh Abdulrahaman Kinana pamoja na kueleza baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa na pande zote likiwemo la kuheshimu uhuru na haki kila mwanachama kugombea nafasi za uongozi wamewataka viongozi hao kuwa na uvumilivu wa  kisiasa.
 
Akihitimisha kikao hicho rais wa Tanzania Mh Dr, Jakaya Kiwete amesema Tanzania itanedelea kutoa mchango wake wa hali na mali wa kupigania amani na kuhakikisha mazungumzo yanatumika kumaliza tofauti popote zinapojitokeza kwani ni jambo linalowezekana.
 
Zoezi la kuhitmisha makubaliano hayo kwa kutiliana sahihi lilitarajiwa kufanyika saa nne hadi saa tano mchana wa tarehe 21/01/2015  lakini  halikuwezekana kutokana na kuibuka kwa mvutano miongoni mwao ambao ulisababisha zoezi hilo kumalizka saa sita na robo usiku.

Wednesday, January 21, 2015

Spika wa Bunge amesema sio jukumu lake kuwaondoa wenyeviti wa kamati za Bunge ambao wanatuhumiwa katika sakata la Escrow.

Spika wa bunge Mh Anna Makinda amesema siyo jukumu lake kuwaondoa wenyeviti wa kamati za bunge ambao wanatuhumiwa katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow isipokuwa wao wenyewe wanatakiwa kutii azimio la bunge namba tatu linalowataka wajiuzulu.
Wakati Mh Makinda akieleza hayo tena kwa kusisitiza kuwa wenyeviti hao tayari wameshajiuzulu baadhi ya kamati ikiwemo ya katiba na sheria ambayo mwenyekiti wake ni Mh William Ngeleja ambaye ni miongoni mwa wabunge wanaotuhumiwa kwenye sakata hilo bado anaendelea na wadhifa huo.
 
Mh Makinda ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kupokea msaada wa vifaa vya Teknohama vilivyotolewa na serikali ya China kupitia balozi wake hapa nchini ambapo amesema vifaa hivyo vitaweza kuokoa zaidi ya bilioni moja ambazo hutumika kuchapisha miswada mbalimbali na taarifa nyingine za bunge badala yake sasa wabunge watakuwa wanatumiwa moja kwa moja kwenye mtandao.
 
Akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya dola za kimarekani laki moja balozi wa china hapa nchini Lu Youqing amesema vifaa hivyo ni ahadi aliyoitoa rais wa China wakati wa ziara yake hapa nchini ambapo alimwahidi spika wa bunge Mh Makinda na kuongeza kuwa china imewekeza zaidi ya dola bilioni 3.1 hasa sekta ya kilimo na viwanda na kwamba kuna kampuni zaidi ya 500 zinazomilikiwa na wachina ambazo zimetoa ajira kwa watanzania laki moja.

Zanzibar kupata madaktari bingwa - Shein


  Baadhi ya washiriki wa mkutano huo

..............Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar iko katika juhudi za   kuhakiksiha   inakuwa na madaktari bingwa wa fani mbalimbali wakiwemo wanaohusiana na maradhi  ya mfumo wa utoaji wa haja ndogo  katika kipindi kufupi kijacho.
Dr. Shein ametoa ahadi hiyo wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa wataalamu wa maradhi  yanayohusiana na  mfumo wa utoaji  haja ndogo  kutoka Uingereza ambao kwa mwaka huu wameamua kufanya mkutano mkuu hapa zanzibar.
Mkutano huo unaofanyika mkoa wa Kusini Unguja ambapo Dk Shein  amesema serikali yake imepania  na ndio maana imewekeza zaidi katika vyuo vya afya na  kuweka mitaaala maalum katika chuo kikuu cha Zanzibar lengo likiwa ni kupunguza hali ya sasa ambapo daktari mmoja anatibu watu 9700.
Naye Dkt Roger Plail akizungumza kwa niaba ya wataalamu wenzake amesema wataendeleza ushirikaino na madaktari wa  Zanzibar  ambao ndiyo uliowafanya waamue kufanya mkutano  wao Zanzibar.
Katika mkutano huo ambao pia unahudhuriwa na wataalmu wa Zanzibar na Tanzania bara mada mbalimbali ziliweza kujadaliwa na wataaalmu hao..
Mmoja katika magonjwa ambayo  hivi sasa yanaonekana kuzidi kwa kasi hapa nchini ni matattizo ya utoaji wa haja ndogo na kuwepo kwa mkutano huu ni moja ya mikakati ya seriklai  kutafutia dawa  tatizo  hilo.

Monday, January 19, 2015

Muhtasari wa habari

Lema, Nassari wadai watamtoa Muhongo bungeni kwa mabavu. Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika Viwanja vya Relini mjini Moshi, Lema alisema Januari 27 mwaka huu ataingia bungeni akiwa na lengo moja tu la kumtoa kwa mabavu, Profesa Muhongo.

Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless Lema amesema atamtoa kwa mabavu bungeni Waziri wa nishati na madini,Profesa Sospetre Muhongo katika kikao kijacho cha Bunge endapo atakuwa hajaondolewa kwenye nafasi hiyo.

Mkakati huo wa Lema umeungwa mkono na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ambaye pia amepanga kumtoa bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Cheng

Saturday, January 17, 2015

Baadhi ya matokeo ya ligi kuu ya uingereza jion hii ya leo

#BPL RESULTS:
Swansea 0-5 Chelsea, Aston Villa 0-2 Liverpool, 0-2 Manchester United, Spurs 2-1 Sunderland, Burnley 2-3 Crystal Palace, Leicester 0-1 Stoke #SSFootball

Friday, January 16, 2015

Watumishi watatu wa serikali wapandishwa kizimbani.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru imewafikisha mahakamani watumishi watatu wa serikali akiwemo mkurugenzi wa fedha wa benki kuu ya Tanzania BOT Julius Angelo kwa tuhuma za kupokea rushwa ya zaidi ya shilingi bilioni 1.8 ambazo ni sehemu ya fedha za Escrow.
Watuhumiwa hao wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu,jijini Dar es Salaam ambapo mara baada ya kusomewa mashitaka yao mahakama imetoa zuio la matumizi ya fedha hizo hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa hukumu na hilo limekuja baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo kutoa zuia hilo.
 
Mtuhumiwa wa kwanza ni Julius Angelo mkurugenzi wa fedha wa benki kuu ya Tanzania BOT ambaye waendesha mashitaka kutoka Takukuru Leornad Swai na Marx Ari wamedai mbele ya hakimu mkazi Devota Kisoka wa mahakama hiyo kuwa Angelo anatuhumiwa kwa shtaka la kupokea rushwa ambapo februari 06 mwaka jana, akiwa jengo la benki ya mkombozi alipokea sh. Milioni 161.7 kupitia akaunti yake.
 
Waendesha mashitaka hao wameieleza mahakama kuwa Angelo alijipatia fedha hizo kutoka kwa James Rugemalira ambaye ni mkurugenzi wa Engineering and Marketing Ltd vip na ambaye pia alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited IPTL, kama tuzo ya kusaidia kuidhinisha malipo kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP.
 
Mtuhumiwa huyo amekana shitaka hilo na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili watumishi wa serikali watakaosaini bondi ya sh. Milioni 50 kila mmoja na yeye kutakiwa kutoa sh milioni 80 taslim au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hizo masharti aliyoshindwa kutimiza na kupelekwa rumande hadi januari 27 mwaka huu upande wa mashitaka utakapoanza kutoa maelezo ya awali.
 
Mshitakiwa mwingine ni Stephen Urassa ambaye ni mwanasheria wa shirika la umeme nchini Tanesco ambaye mbele ya hakimu Janeth Karienda waendesha mashitaka hao wa Takukuru wamedai kuwa mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kosa la kuomba na kupokea rushwa ya sh milioni 161.7 kwa Rugemalira kama tuzo kwa kuiwakilisha Tanesco na kampuni nyingine zilizokuwa zimeingia mkataba shirika hilo, yuko nje kwa dhamana hadi feb 11 mwaka huu baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
 
Mtuhumiwa mwingine ni Kyabukoba Mutabingwa ambaye ni meneja misamaha ya kodi TRA na anatuhumiwa kwa makosa manne ya kupokea rushwa ya zaidi ya sh. Bilioni 1.4 ambapo alikuwa anaiwakilisha tra pamoja na kampuni ya mabibo wine ambapo waendesha mashitaka hao wamedia mbele ya hakimu Janeth kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo jan 27 mwaka jana ambapo alipokea bilioni 1.6 mwezi huohuo milioni 161.7 na julai 15 alipokea sh milioni 161.7 novemba 14 alipokea sh milioni 161.7.
 
Aidha mtuhumiwa huyo ametakiwa kuwa na wadhamini watatu wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya shilingi milioni 340 na yeye atoe fedha taslim sh bilioni 1 na ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa rumande hadi jan 29 mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena kwa maelezo ya awali.

PAC yabaini upotevu wa fedha zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 mamlaka ya Bandari TPA.

Kamati ya bunge ya hesabu za serikali PAC imebaini upotevu wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.5 za mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA ambazo zimetumika lakini nyaraka zake hazionekani huku ikiuagiza uongozi wa mamlaka hiyo kuhakikisha fedha zote za nyongeza ya posho za safari walizolipwa watumishi tangu mwaka 2011 kabla msajili wa hazina hajathibitisha zinarudishwa.
Mwenyekiti wa kamati ya PAC Mh Zitto Kabwe ametoa agizo hilo wakati kamati yake ilipokutana na bodi na uongozi wa TPA baada ya kukagua vitabu vyake vya mahesabu ambapo amesema licha ya kiwango cha posho zilizolipwa kuwa kikubwa lakini waliharakisha kujilipa kabla msajili wa hazina hajathibitisha ambapo afisa wa ngazi ya juu alilipwa shilingi laki tano kwa siku kwa safari ya ndani ya nchi na ya nje ya nchi dola za kimarekani mia nane.
 
Akizungumzia suala la ukosefu wa nyaraka za fedha ambazo tayari zimeshatumika makamu mwenyekiti wa PAS Mh.Deo Philikonjombe amesema tatizo hilo limekuwa sugu kwa taasisi mbalimbali za serikali hali inayoashiria kuwa kuna baadhi ya wakurugenzi na watumishi wanafuja fedha za umma kinyume na taratibu na wanapobanwa wanapeleka nyaraka ambazo wakati mwingine ni za kufoji.
 
Kaimu mkurugenzi mkuu wa TPA na mhasibu wake mbali na kukiri upotevu wa nyaraka hizo wamedai kuwa tatizo hilo limetokana na uhifadhi wa nyaraka ambao hadi leo nyaraka nyingi za TPA zinahifadhiwa kwenye karatasi na kuiahidi kamati hiyo kuwa wataziwasilisha mwisho wa mwezi wa mwezi febuari mwaka huu hali iliyozua maswali mengi kwa wajumbe wa kamati hiyo kuwa watazipata wapi kama kipindi chote hicho hazijaonekana.

Thursday, January 15, 2015

UDSM kwa kushirikiana na ITV/Radio One wakubaliana kuandaa midahalo ya Urais.

 
Jumuiya ya wanataaluma wa chuo kikuu cha Dar es salaam kwa kushirikiana na  ITV/REDIO ONE wamekubalianan kuandaa  midahalo ya wagombea urais kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambapo itv/redio one watakuwa wanarusha midahalo hiyo mja kwa moja.
Makubalinia hayo yamefanyika jijini dar es salaam baina ya  mkurugenzi mtendaji  wa ITV/Redio One Joyce Mhavile na mwenyekiti wa udasa Profesa Kitilya Mkumbo ambapo mwenyekiti  huyo amesema uwepo wa midahalo hiyo ni  nafasi nzuri kwa wagombea kunadi sera  zao.
 
Kwa upande wake mkurugenzi wa ITV /Redio One amesema wao kama kityo cha  habari wanaamini midahalo hiyo ni  nguzo imara kwa wasomi kuweza kuchambua  hoja za wagombea kabla ya kufanya maamuzi ya kuwachagua ama la,Kama  ilivyo ada katika mikutano baadhi ya waandishi w habari walipata nafasi ya kuuliza  maswali mbalimbali na kupatiwa  majibu  na meza kuu.
 

Friday, January 09, 2015

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr. Reginald Mengi amesema juhudi, akili hukwamua watanzania.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr. Reginald Mengi amesema iwapo serikali itaandaa mazingira mazuri vijana na Watanzania kwa ujumla wanaweza kujikwamua kiuchumi kwa kutumia akili, juhudi,  na utajiri wa raslimali za taifa.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP DR Reginald Mengi ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizindua shindano jipya la kubuni Wazo la Biashara litakaloendeshwa kwa miezi sita mfululizo kuanzia Januari 2015, na kila mwezi mshindi mmoja atajishindia zawadi ya shilingi milioni 10 atakazozitumia kama mtaji wa kutekelezea kwa vitendo wazo lake la biashara.
 
Amesema Shindano hilo linalojulikana kama 3N ikiwa ni kifupisho cha ‘NITABUNI biashara, NITATEKELEZA na NITAFANIKIWA’, litawashirikisha Watanzania pekee na litaendeshwa kwa njia ya mtandao wa kompyuta ambapo mshiriki anatakiwa atatume wazo lake kwa anuani ya twita @regmengi shindano la wazo la biashara.
 
Katika kupata mshindi, jopo maalum la wataalamu watapitia mawazo yatakayowasilishwa na kuteua mawazo 10 bora, na watunzi wa mawazo hayo 10 watafanyiwa usaili kwa njia ya simu ili jopo lijiridhishe kuwa mawazo waliyotoa ni yao binafsi na jinsi walivyojiandaa kuyatekeleza kibiashara. Jopo la wataalamu litamteua mshindi baada ya usaili huo.